SASA ni saa tu zimeanza kuhesabika kabla ya mabingwa Yanga kushuka dimbani kukipiga na watani wao, Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, keshokutwa Jumapili.
Yanga SC.
Iwapo Simba ambao ni wenyeji watapoteza, itakuwa ‘noma sana’, maana watakuwa wameshindwa kulipa kisasi cha msimu uliopita, lakini Yanga pia ikifungwa, itakuwa ‘noma sana’, maana itazidiwa pointi sita na watani wake hao, si chache.
Mengi yanayozungumzwa kuelekea mchezo huo, kikubwa ni tambo za mashabiki wa kila upande ambapo wale wa Simba wanaamini Amissi Tambwe lazima awalize Wanajangwani hao, ambao nao wanaamini lazima Mrisho Ngassa awanyamazishe Msimbazi kama alivyoahidi.
Simba SC.
Tambwe atishiwa kuuawa
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum, Tambwe ambaye anaongoza kwa mabao katika ligi hiyo akiwa amefunga nane, amesema amekuwa akipigiwa simu kutoka kwa watu asiowajua wakimwambia ole wake aifunge Yanga, atakiona cha moto.
“Nimeshangaa sana hapa Tanzania watu wanavyoishi, nimekuwa nikipokea simu hizo mara kwa mara na wote wakinitishia kuniua kama nitaifunga Yanga, ukiwauliza wanasema tena kifo changu kitatokana na risasi, kama nataka usalama wangu basi nihakikishe siwafungi Yanga,” alisema Tambwe na kuongeza:
“Nimeshindwa kuwatambua kwa kuwa namba zao hazionekani (private number) kwenye simu yangu, wanaweza kuona kama nitaogopa vitisho hivyo, lakini nakwambia hali hiyo haiwezi kunizuia kufanya kazi yangu, nikipata nafasi nitafunga kama kawaida yangu, hii ndiyo kazi yangu.”
Tambwe amshangaa Ngassa
“Lakini kufunga ni mipango ya Mungu, nimesoma gazeti moja (Championi), nikaona mtu ameongea kitu cha ajabu kidogo, ni vizuri kujiwekea malengo lakini siyo kusema eti nisipofunga nitachoma moto nyumba zangu, nadhani hakutakiwa kutamka maneno hayo, amekosea sana,” alisema Tambwe.
Kauli hiyo ya Tambwe inakuja kufuatia Ngassa, kutamka kuwa atahakikisha anawafunga Simba au kutoa pasi itakayozalisha bao na kama atashindwa kufanya hivyo katika mechi hiyo, yupo radhi kuchoma moto nyumba zake tano zilizopo Dar na Mwanza.
Ngassa anawaza kufunga tu
Akizungumzia mechi hiyo, Ngassa alisema hana mawazo ya kuwa mfungaji bora lakini nia yake ni kuhakikisha Yanga inaibuka na ubingwa msimu huu huku yeye akifanya kazi yake inavyotakiwa.
“Akili na malengo yangu hivi sasa ni kuhakikisha Yanga inatwaa ubingwa, ninachotaka ni kufanya suala la ufungaji linakuwa lazima kwangu katika mechi zote na kama sitafunga basi nitoe pasi ya bao,” alisema Ngassa.
Maoni ya makocha
Kocha Hemed Morocco aliyemaliza mkataba wake na Coastal Union, amesema: “Ninaipa asilimia tisini Yanga kwa sababu ina muda kidogo ipo na wachezaji walewale, Simba bado inajipanga,” alisema Morocco.
Kuhusu mwamuzi wa mechi hiyo, Israel Nkongo, Mwenyekiti wa Matawi wa Vijana wa Yanga, Bakili Makele alisema: “Tunampa onyo na kumtaka mwamuzi kuchezesha kwa kufuata kanuni zote kumi na saba za soka, maana wapinzani wetu wamekuwa wakifunga mabao mengi kwa njia ya penalti, wanapata penalti zisizo za msingi.”
Upande wa Simba, Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alipozungumza na gazeti hili alisema: “Tunampongeza mwamuzi kupata nafasi ya kuchezesha mechi hiyo lakini tunamtaka ahakikishe anafuata sheria zote za soka, mechi hii inaweza kumjenga au kumbomoa.”
Nondo Aonesha Alipotupwa, Asimulia Sakata Zima la Kutekwa "Ukisema
Tutakupiga Risasi"
-
Nondo Aonesha Alipotupwa, Asimulia Sakata Zima la Kutekwa "Ukisema
Tutakupiga Risasi"
47 minutes ago
0 comments:
Post a Comment