Thursday, October 17, 2013

MCHEZO mzima wa namna wahamiaji haramu 16 raia wa Somalia na Ethiopia waliokamatwa Jumamosi iliyopita mjini hapa umegundulika.
Watu hao walikamatwa wakiwa hoi baada ya kukosa hewa katika barabara kuu iendayo Iringa jirani na baa maarufu ya Mzuwanda, baada ya raia wema kuwapenyezea siri maofisa uhamiaji waliokuwa eneo la Msamvu.
Habari zilizopatikana eneo la tukio zinasema kwamba, lori hilo lenye namba za usajili T 707 CGY lilikuwa likitokea Ulolo, Tanga likielekea nchi za Zambia na Afika Kusini.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Godrfey Chambo aliliambia Amani kuwa, akiwa Msamvu na rafiki zake, walishangaa kuona mtu mwenye asili ya Somalia akidondoka kwenye lori ndipo walipoamua kufuatilia na kutoa taarifa kwa maofisa wa uhamiaji.
“Sisi tulikuwa na mishe zetu pale Msamvu, mara nikashangaa mtu anadondoka akiwa hoi, amechafuka na kitu kama unga, kumbe ni chokaa. Lile gari lilikuwa linajaza mafuta pale. Nikamwambia mwenzangu ndipo tukaamua kutoa taarifa kwa maofisa wa uhamiaji.
“Dereva alionekana kushtukia mchezo, alipomaliza kujaza mafuta, akaliondoa gari kwa kasi. Watu wa bodaboda wakaanza kulifukuza hadi walipokamatwa kule Mzuwanda,” alisema Chambo.
Jeshi la polisi mjini hapa kwa kushirikiana na watu wa uhamiaji baada ya kukamata gari hilo walikwenda nalo hadi Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa na kuwatoa wahamiaji hao ambapo wengine walifikishwa hospitalini kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Mmoja wa maofisa wa uhamiaji mkoa wa Morogoro, Wilfred Minja, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao ambapo pia aliwashukuru raia wema kwa ushirikiano walioutoa wenye lengo la kulinda usalama wa nchi yetu.

0 comments:

Post a Comment

Other blogs

Copyright ©2013 Gabriel Fredy . Powered by Blogger.

Total Pageviews

GABRIEL FREDY

SELECT LANGUAGE

DIEGO COSTA'S GOAL ON CHELSEA

Popular Posts